Monday, May 23, 2011

SIKU YA KIAMA


SIKU YA KIAMA
Ya kiama katabiri                       Dunia ‘ta tamatika
Kwa hamu tukasubiri                 Siku hiyo kihakika
Wengine wakahubiri                  Bwana yesu atashuka
Sijitupe kwa kaburi                   Wenzako watateseka

Siku hiyo ni ya siri                     La kwako ni kuokoka
Ombea wenzako heri                Wasije wakateseka
Usiisambaze habari                   Eti mwisho keshafika
Sijitupe kwa kaburi                   Wenzako watateseka

Siliuze lako gari                         Matope utajipaka
Utapandwa nayo mori               Wenzako wakikucheka
Siogope  kufikiri                        Majukumu kujitwika
Sijitupe kwa kaburi                   Wenzako watateseka

Thursday, May 12, 2011

MVUA HII WANITISHA


MVUA HII WANITISHA
Kibaridi chaniweza                 Ni mvua ilonyesha
Sitaki kufukuza                       Hata kama wanitisha
Tangu nane wajikaza               Ni jioni bado tosha
Taka hadi kuwe giza               Ndipo hasa jikomesha

Matope wayaongeza               Na viatu wazeesha
Ni furaha wanitoza                 Ta ingawa wanilisha
Wako mwenendo punguza     Matembezi kuyapisha
Nakuomba we tuliza               Ndiposa usije chosha

Mi sitaki nije cheza                 Ukulima Wadumisha
Sitaki njaa kujilaza                  Sababu kukufurusha  
Naomba kunisikiza                  Hali hewa imarisha
Usije ukaniliza                        Cha ukoka kunivisha

Wednesday, May 11, 2011

TEKNOLOJIA NI NJEMA


TEKNOLOJIA NI NJEMA
Tumeipenda tovuti            Makazini manyumbani
Kufanyia utafiti                 Hata kwetu masomoni
Ndio wa mgongo uti         Kiuchumi kwetu nchini
Teknolojia ni njema          Ikitumiwa ipasavvyo

Tukiwashe kiberiti            Tujitie mpangoni
Tuikaze na boriti               Wakosao tumaini
Tuzisome ripoti                 Toka mtandaoni
Teknolojia ni njema          Ikitumiwa ipasavvyo


Jamani tusiketi                  Eti ni ya uzunguni
Tulivalie kabuti                 Tuelekee mwezini
Tusijifunge kwa neti          Tujikaze kisabuni
Teknolojia ni njema          Ikitumiwa ipasavvyo

TAIFA LETU TULIENZI


TAIFA LETU TULIENZI
Najitwika jukumu            Kuendeleza taifa
Nifahamu umuhimu          Wa kuipa nchi sifa
Nibaki kutabasamu         Kazini kimaarifa
Taifa letu tulienzi              Ndio Kenya twajivunia

Usikazie tabasamu          Ukiketi kwenye sofa
Bora chukua zamu           Endelea kimaarifa
Sisubiri mwenza hamu     Kutawale kwa masafa
Taifa letu tulienzi              Ndio Kenya twajifunia

Kaditamati imetimu        Nimeipokea arafa
Kwa yangu ndogo simu   Nahitajika kama refa
Niichezeshe kihakimu    Nchi yangu kama Fifa
Taifa letu tulienzi ndio    Kenya twajivunia

Monday, May 9, 2011

TUJIKAZE KISABUNI


Maisha ni magumu          Tutahepa kwenda wapi
Hatuwezi kujikimu           Tutajibu swali lipi
Serikali twalaumu            Uwezo wetu ni upi
Tujikaze kisabuni              Tujiinue kiuchumi

Tumbo zetu sitajaa          Kijikaza kisabuni
Tusilale kwa mataa          Vya bure kungojani
Hata kama ni sanaa         Tuitilie manani
Tujikaze kisabuni              Tujiinue kiuchumi